Mwanamke na Uongozi
Miaka ya nyuma nchini Tanzania, wanawake hawakuwa wakipewa kipaumbele katika uongozi. Hata hivyo, hivi karibuni serikali na jamii zimetambua mchango wa wanawake, na hivyo kuanza kuwapa nafasi mbalimbali za uongozi, si tu serikalini bali pia katika taasisi zisizo za kiserikali.
Hata hivyo, bado wapo baadhi ya watu wanaoamini kuwa wanawake hawawezi kushika nyadhifa za uongozi kutokana na changamoto wanazokumbana nazo. Wengi wa watu hawa hawajui kuhusu Mtawala wa kike aliyerithi uchifu baada ya baba yake kufariki dunia.
Leo, kalamu yangu inawaandikia juu ya Mwami Theresa Ntare VI, aliyezaliwa mwaka 1926 na kufariki mnamo tarehe 23 Mei 1993 akiwa na umri wa miaka 67. Theresa alikuwa mtawala wa kike aliyerithi uchifu baada ya baba yake, Mwami Gwasa, kufariki dunia. Alikabidhiwa uchifu kwa sababu hakuwa na kaka wa kurithi nafasi hiyo katika familia yao. Kinyume na mila zilizotaka kutafutwa mtoto wa kiume kutoka kwa ndugu wengine, Bi. Theresa alipewa nafasi hiyo, na hivyo kuwa chifu wa kwanza mwanamke katika jamii ya Waha.
Akiwa na umri wa miaka 19, Bi. Theresa alianza kutawala chini ya usimamizi wa mama yake hadi alipofikia umri wa kutosha kuchukua majukumu kamili ya uongozi.
Bi Theresa ni nani hasa?
Kwenye chapisho la “WHO’S WHO IN EAST AFRICA,” 1963-1964, Bi. Theresa Ntare anaelezewa kama kiongozi wa kipekee. Alizaliwa Tanganyika mwaka 1926 na alisoma katika Shule ya Wasichana ya Tabora kuanzia mwaka 1942 hadi 1946. Mwaka 1959 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Kasulu, na mwaka 1962 aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo na Utamaduni. Hata hivyo, mwaka 1965 alikataa kugombea ubunge na kuendelea na shughuli zake nyingine.
Mnamo mwaka 1960, Bi. Theresa alikuwa mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria (LEGICO) na pia mwenyekiti wa kwanza wa Muungano wa Machifu wa Tanganyika. Baadaye alihudumu kama mmoja wa wanadiplomasia wa nchi. Alishirikiana na Mwalimu Julius Nyerere kudai uhuru kwa kueneza chama cha TANU katika maeneo ya Kigoma na Rukwa, akiwa na ushawishi mkubwa. Pia, alishirikiana na Chifu Abdala Fundikila kueneza TANU katika Mkoa wa Tabora.
Bi. Theresa alikuwa na wadogo zake wawili, Mary Gwasa na Anna Gwasa. Anna alikuwa mwanachama wa TANU aliyesaidia dada yake kueneza chama hicho na kufanikisha uhuru wa Tanganyika. Baada ya uhuru, Anna aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya wa kwanza mwanamke.
Katika maisha ya ndoa, Bi. Theresa aliolewa na Bwana George Shinganya, na walibahatika kupata watoto wanane: Costa, Martin, Joseph, Maximilian, Elizabeth, Wivina, Nestory, na Lucy. Hata hivyo, ndoa yao ilivunjika, na baada ya kutengana, Bi. Theresa alihamia Dar es Salaam. Baadaye, aliolewa na Chief Luis Dantes Ngua wa Sumbawanga, ambaye aliachana na wake zake wengine baada ya kumuoa Bi. Theresa. Katika ndoa hiyo, walipata mtoto mmoja wa kike, Flora Ngua.
Pamoja na mafanikio yake makubwa, Bi. Theresa alikumbana na changamoto nyingi. Mfumo dume ulikuwa mojawapo ya changamoto kuu, kwani jamii nyingi zilikuwa zimezoea kuwa na watawala wa kiume. Alilazimika kujitahidi sana ili kukubalika kama mtawala wa kike kwa kuonyesha uwezo wake wa kipekee katika uongozi.
Nini Tunajifunza
Kuna mengi ya kujifunza kutoka kwa Bi. Theresa Ntare. Kama mtawala wa pekee wa kike Tanzania, alitumia nafasi yake kutetea haki za wanawake, haswa katika elimu, kujitegemea, na kujiamini. Alisimamia watoto wake kwa bidii, akihakikisha wanapata elimu bora.
Bi. Theresa alituonyesha kuwa wanawake wanaweza kuwa viongozi bora, wakichanganya jukumu la uongozi na maisha ya kila siku. Aliwahamasisha wanawake kujiamini na kutafuta nafasi mbalimbali za uongozi licha ya changamoto za kimfumo.
Leo hii, tukiwa na idadi kubwa ya viongozi wanawake katika mihimili yote ya serikali, tunapaswa kuendeleza juhudi hizi. Ni jukumu la kila mzazi kuwaandaa watoto wao kwa uongozi wa baadaye. Pia, ni wakati wa jamii kuondokana na fikra potofu kuhusu wanawake. Sote tumeumbwa sawa, tuna haki sawa, na yeyote anaweza kushika nafasi yoyote ya uongozi.
Comments
Post a Comment